Thursday, 21 August 2014

CCM YASISITIZA MCHAKATO WA KATIBA UENDELEE.




Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sekretarieti Makao Makuu ya CCM Dodoma.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Dodoma ,Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi alisema,
Kamati Kuu pamoja na mambo mengine, ilipokea taarifa na kufanya tathimini juu ya maendeleo ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini, ndani na nje ya Bunge.

Kamati Kuu vilele imepokea na kujadili taarifa kuhusu mazungumzo na mashauriano kati ya vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR-MAGEUZI na CCM. Mazungumzo ambayo yalisimamiwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini.

Aidha Kamati Kuu ilipokea pia taarifa ya kikao cha Baraza la Vyama vya siasa na pia taarifa ya kikao cha Kituo Cha Demokrasia nchini (TCD). Vikao hivyo vyote vilihusu maendeleo ya mchakato wa Katiba nchini.

Kuhusu mwenendo wa Bunge la Katiba, Kamati Kuu imearifiwa maendeleo ya majadiliano na upigaji kura katika kamati za Bunge hilo. Kwa ujumla Kamati Kuu imeridhishwa na namna wajumbe wa Bunge Maalum wanavyoshiriki katika kujadili na kujenga hoja na wanavyoshughulikia tofauti za kimtazamo na kimawazi katika vikao vyao na hatimaye uhutimishaji wa majadiliano kwa kura.

Kamati Kuu inawahimiza wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kuhudhuria vikao vya kamati na vile vya Bunge na kushiriki katika mijadala kwa kutanguliza masilahi mapana ya taifa na hatimae kuipatia nchi katiba inayotarajiwa na watanzania wote. Chama Cha Mapinduzi kinautakia kila lakheri mchakato huu.


Aidha Kamati Kuu imeridhishwa na juhudi za vyama na wadau mbalimbali katika kujenga na kuimarisha maridhiano na mshikamano kwa lengo la kupata muafaka. Hata hivyo Kamati Kuu imesikitishwa na kuvunjika kwa mazungumzo kati ya CCM, CUF,CHADEMA na NCCR-MAGEUZI yaliyokuwa yanasimamiwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini kwa kengo la kujenga na kuimarisha maridhiano na mshikamano ili kupata muafaka.

Kamati Kuu imepokea na kuridhishwa na taarifa kuhusu juhudi zinazofanywa na Kituo Cha Demokrasia nchini (TCD) pamoja na vyama vinavyounda TCD katika kutafuta muafaka wa kisiasa kwa lengo la kuimarisha amani, utulivu, mshikamano na kuaminiana kati ya wadau mbalimbali na hasa kati ya vyama vya siasa.

Kamati Kuu inaunga mkono juhudi za TCD za kuendeleza mashauriano kati ya vyama na ndani ya vyama kwa lengo la kupunguza mivutano, kujenga uaminifu na ustahimilivu na umoja kati yao.

Hivyo Kamati Kuu imempongeza Katibu Mkuu wa CCM kwa namna alivyoshiriki na kukiwakilisha Chama kwenye vikao hivyo.

Kamati Kuu imemuagiza Katibu Mkuu aendelee kukutana na vyama na wadau wengine katika kufanikisha lengo la maridhiano hayo.

Mwisho Kamati Kuu inaendelea kuwasihi Watanzania wote kuendelea kushikamana na kuvumiliana pale wanapopishana kimtazamo juu ya hoja mbalimbali za katiba kwani Amani, Utulivu na Utanzania wetu ni muhimu kuliko tofauti zetu za kimitazamo. Mchakato wa Katiba nchini uendelee kuwa fursa ya kuijenga nchi yetu badala ya kutumika kutugawa na kututenganisha.

MIMI SI KIKWAZO CHA MAHUDHURIO KWENYE KAMATI ZA BUNGE LA KATIBA- RAIS KIKWETE




Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiagana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi kabla ya kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati kuu ya chama hicho juzi. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama. Picha na Ikulu

Dodoma:

Katika kile kinachoonekana kutaka mawaziri washiriki vikao vya kamati za Bunge la Katiba ili kukidhi matakwa ya akidi, Rais Jakaya Kikwete amesema hakuna ulazima wa mawaziri kuambatana naye kwenye ziara zake mikoani, badala yao wawepo makatibu wakuu wa wizara kama wanahitajika.

Rais Kikwete alinukuliwa akisema ndani ya Kamati Kuu ya CCM iliyomaliza kikao chake juzi mjini hapa kwamba yeye si kikwazo cha mahudhurio kwenye kamati za Bunge hilo na kwamba hata katika ziara yake ya Morogoro hawahitaji.


“Mwenyekiti aliweka wazi kabisa kwamba hata katika ziara yake ya Morogoro watumwe makatibu wakuu wa wizara kama kuna ulazima huo,” kilisema chanzo chetu.


Hata hivyo, katika ziara yake mkoani Morogoro iliyoanza jana, Rais Kikwete aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani ambaye pia ni Mbunge wa Ulanga Mashariki ziara hiyo ilikoanzia.


Pia alikuwapo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele ambaye alihudhuria tukio la uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini katika Kijiji cha Mwaya.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema: “Kamati Kuu inawahimiza wajumbe wa Bunge la Katiba, kuhudhuria vikao vya kamati na vile vya Bunge na kushiriki katika mijadala kwa kutanguliza masilahi mapana ya Taifa na hatimaye kuipatia nchi Katiba inayotarajiwa na Watanzania wote.


Akifafanua, Nnauye alisema suala la mahudhurio kwenye vikao lilizungumzwa kwenye CC na kwamba mawaziri na wajumbe wengine wa Bunge la Katiba, wametakiwa kupunguza utoro ili akidi ya wajumbe iwe inatimia wakati wa kufanya uamuzi.


Nnauye alisema tatizo la wabunge na mawaziri watoro katika vikao vya kamati linajulikana hata ndani ya CCM... “Sasa ni wakati wa kuwaambia kuwa wapunguze kazi zao nje ya Bunge maana suala la utoro ni kweli linatufikia na wabunge nawasihi sana wasiwe watu wa kutoka-toka wakati vikao vinaendelea,” alisema.


Akidi vikaoni
Suala la akidi limekuwa likikwaza kamati za Bunge Maalumu kiasi cha kusababisha baadhi kuchelewa kuanza kwa vikao na wakati mwingine kuahirishwa.


Kadhalika, baadhi ya ibara kwenye Rasimu ya Katiba zimekuwa zikikosa akidi ya theluthi mbili ya kura kutokana na utoro wa baadhi ya wajumbe, wakiwamo mawaziri ambao mara kadhaa wamelalamikiwa na wenyeviti wa kamati kwa kutohudhuria.


Agosti 18, mwaka huu Kamati namba 11 ililazimika kuweka kando kazi zake na ikafanya kile ilichokiita semina ya uelewa kwa wajumbe, baada ya akidi kutofikiwa.


Kamati hiyo ina wajumbe 52 baada ya kufariki dunia kwa mmoja wa wajumbe wake, Shida Salum Mohamed lakini siku hiyo idadi yao haikuwawezesha kuanza kwa kikao baada ya kupungua kwa wajumbe kadhaa kutoka Zanzibar.


Hiyo ni miongoni mwa kamati zinazoathiriwa na wingi wa mawaziri na naibu mawaziri, wakiwamo Waziri wa Kilimo na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Godfrey Zambi, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kwebwe Steven na Manaibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Adam Malima.


Pia katika kamati hiyo yumo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud na Naibu Waziri wa Mawasiliano Zanzibar, Issa Gavu.


Wengine ni Hawa Ghasia (Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi), Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu), Celina Kombani (Ofisi ya Rais – Utumishi) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Mahadhi Juma Maalim.


Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri wake wa nchi, Mohammed Aboud. Hata hivyo, haikufahamika mara moja kama walikuwa miongoni mwa waliokwaza kikao hicho.


Tatizo la akidi pia lilijitokeza juzi katika Kamati Namba Tatu kiasi cha kumsukuma, Mwenyekiti wake, Dk Francis Michael kuamua kuahirisha kikao saa tano asubuhi hadi saa nane mchana kutokana na kile alichokiita kuwapa muda wajumbe waende kusoma zaidi Sura ya Tisa ambayo inahusu muundo wa Bunge.


Dk Michael alikiri kwamba hadi ilipotimu saa 4:00 asubuhi juzi, kamati yake ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa wajumbe wanne hivyo waliwapigia simu na kubaini kwamba walikuwa katika shughuli nyingine, ikiwamo kumpokea Rais Kikwete uwanja wa ndege.


“Baadhi ya wajumbe ni mawaziri, kwa hiyo baada ya kukamilisha majukumu yao walifika na saa tano hivi akidi ilikuwa imetimia,” alisema Dk Michael.



Na: Mwananchi

RATIBA YA KUUAGA MWILI WA ALIYEKUWA MWENYEKITI MSTAAFU WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI MHE. JAJI LEWIS MAKAME VIWANJA VYA KARIMJEE TAREHE 22 AGOSTI 2014.


                             R.I.P Mhe. Jaji Lewis Makame.
                
MUDA
TUKIO
MHUSIKA
3.00- 3.30 ASUBUHI
WANANCHI NA WATUMISHI KUWASILI
KAMATI YA MAZISHI
3.30 – 4.00 ASUBUHI
VIONGOZI WASTAAFU, MAWAZIRI, MAJAJI WASTAAFU , VIONGOZI WA TUME YA
TAIFA YA UCHAGUZI, SERIKALI, TAASISI NA VYAMA VYA SIASA KUWASILI
KAMATI YA MAZISHI
4.00 -4.15 ASUBUHI
WAH. MAJAJI WA MAHAKAMA KUU KUWASILI
KAMATI YA MAZISHI
4.15 – 4.20 ASUBUHI
MHE. JAJI KIONGOZI

KAMATI YA MAZISHI
4.20 – 4.25 ASUBUHI
MAHAKAMA YA RUFANI KUWASILI
KAMATI YA MAZISHI
4.25 – 4.30 ASUBUHI
JAJI MKUU KUWASILI
KAMATI YA MAZISHI
4.30 – 4.40 ASUBUHI
SPIKA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO KUWASILI
KAMATI YA MAZISHI
4.40  - 4.45 ASUBUHI
MHE. WAZIRI MKUU KUWASILI
KAMATI YA MAZISHI
4.45  - 4.50
ASUBUHI
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUWASILI
IKULU/ KAMATI YA MAZISHI
4.50 – 5.00 ASUBUHI
MHE. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUWASILI
KAMATI YA MAZISHI
5.00 – 5.05 ASUBUHI
MWILI WA MAREHEMU KUWASILI
KAMATI YA MAZISHI


5.05 – 5.10 ASUBUHI
SALA

5.10 – 5.20
WASIFU WA MAREHEMU
MWANAFAMILIA
5.20 – 5.30 ASUBUHI
NENO KUTOKA KWA CHAMA CHA MAJAJI WASTAAFU
MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAJAJI WASTAAFU, MHE. JAJI MIHAYO
5.30 -5.40
NENO KUTOKA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI MHE. JAJI LUBUVA
5.40 -5.50 ASUBUHI
NENO KUTOKA KWA MHE. JAJI MKUU
MHE. JAJI MOHAMED CHANDE OTHMAN
5.50 – 6.00 ASUBUHI
NENO KUTOKA KWA MHE. RAIS
MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE
6.0 -6.10 MCHANA
NENO LA SHUKURANI
MSEMAJI WA FAMILIA
6.10 MCHANA 6.50 MCHANA
KUAGA
KAMATI YA MAZISHI
6.50 -7.00 MCHANA
KUWASILI KANISANI – ST. ALBAN - UPANGA
KAMATI YA MAZISHI
7.00 MCHANA  - 9.00 ALASIRI
MISA YA KUMUOMBEA MAREHEMU

9.00 ALASIRI
KUONDOKA KUELEKEA MUHEZA - TANGA
KAMATI YA MAZISHI

Wednesday, 20 August 2014

RAIS KIKWETE AWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA DARAJA LA KILOMBERO.



Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipungia wananchi kwa furaha wakati akielekea ukingoni mwa Mto Kilombero kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la kudumu juu ya mto Kilombero Agosti 20, 2014. Anaoongozana nao ni pamoja na Waziri wa Ujenzi Dkt John Pombe Magufuri (kushoto kwa Rais), Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mbunge wa Ulanga Mashariki Mhe. Celina Kombani (kulia), Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera (kushoto) na Mama Salma Kikwete (nyuma ya Rais)
 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akishangiliwa baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la kudumu juu ya mto Kilombero Agosti 20, 2014. Pamoja naye ni Waziri wa Ujenzi Dkt John Pombe Magufuri (kushoto kwa Rais), Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mbunge wa Ulanga Mashariki Mhe. Celina Kombani (kulia), Mbunge wa Mama Salma Kikwete (nyuma ya Rais), Mbunge wa Ulanga Magharibi Dkt Haji Ponda (kulia) na Mbunge wa Kilombero Mhe Abdul Mteketa (kulia kwa Rais)
 
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo toka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Bw. Patrick Mfugale juu ya ujenzi wa daraja la kudumu juu ya mto Kilombero Agosti 20, 2014. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi Dkt John Pombe, Magufuri akifuatiwa
Mama Salma Kikwete.

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la kudumu juu ya mto Kilombero wilayani Kilombero mkoa wa Morogoro Agosti 20, 2014
 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la kudumu juu ya mto Kilombero wilayani Kilombero mkoa wa Morogoro Agosti 20, 2014

 

Magari yakivuka juu ya daraja la muda la Mto Kilombero lililojengwa kurahisisha kazi za ujenzi wa daraja la kudumu katika wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro, wakati wa sherehe za uwekaji jiwe la msingi wa ujenzi wa darajan hilo na Rais Jakaya Mrisho Kikwete Agosti 20, 2014.
 

Magari yakivuka juu ya daraja la muda la Mto Kilombero lililojengwa kurahisisha kazi za ujenzi wa daraja la kudumu katika wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro, wakati wa sherehe za uwekaji jiwe la msingi wa ujenzi wa darajan hilo na Rais Jakaya Mrisho Kikwete Agosti 20, 2014.
 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akijaribu madawati mapya ya shule ya msingi ya Epauko wilayani Mahenge baada ya shule hiyo kukabidhiwa msaada wa madawati 500 na Kampuni ya Kibaran Resources Ltd inayojishughulisha na uchimbaji wa madini aina ya Graphite na Nickel mkoani wa Morogoro Agosti 20, 2014.
 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete na mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi ya Epauko wilayani Mahenge baada ya shule hiyo kukabidhiwa msaada wa madawati 500 na Kampuni ya Kibaran Resources Ltd inayojishughulisha na uchimbaji wa madini aina ya Graphite na Nickel mkoani Morogoro Agosti 20, 2014

PICHA NA IKULU.


Tuesday, 19 August 2014

KIKAO CHA HALMASHAURI KUU YA CCM CHAFANYIKA DODOMA.


Mwenyekiti wa CCM Taifa,Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiingia kwenye ukumbi wa NEC Dodoma ,akiongozana na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana tayari kuongoza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mjini Dodoma.


Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwenye ukumbi wa NEC ,Makao Makuu ya CCM Dodoma.


Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Dk.Maua Abeid Daftari akijadiliana jambo na mjumbe mwenzake Samia Suluhu Hassan muda mfupi kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa hakijaanza kwenye ukumbi wa NEC mjini Dodoma



 Katibu wa NEC Oganizesheni Dk.Mohamed Seif Khatibu akizungumza na Mjumbe wa Kati Kuu ya CCM DK. Salim Ahmed Salim ndani ya ukumbi wa mkutano wa White House kabla ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.



 Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM wakijadiliana kabla ya kuanza kwa kikao kwenye ukumbi wa NEC mjini Dodoma, kutoka kushoto ni Profesa Anna Tibaijuka, Katibu wa NEC Uchumi na Fedha Zakia Meghji na Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Dk. Asha-Rose Migiro.


Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) Mwigulu Nchemba akizungumza na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye kabla ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika Dodoma.

RAIS JAKAYA KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI KUFUATIA KIFO CHA JAJI MAKAME.


    
                               Marehemu Jaji Lewis Makame Enzi ya uhai wake

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, National Electoral Commission (NEC) kufuatia taarifa za kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Lewis Makame kilichotokea katika Hospitali ya AMI Trauma Centre Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Agosti, 2014.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania na Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) chini ya Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, Mheshimiwa Lewis Makame ambaye amelitumikia Taifa letu katika Utumishi wa Umma kwa uaminifu, uadilifu, bidii na umahiri mkubwa”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika Salamu zake.

Katika utumishi wake, Marehemu Jaji Lewis Makame, enzi za uhai wake, alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kabla ya kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa na baadaye Mwenyekiti wa NEC ambayo aliiongoza kwa miaka 17 mfululizo hadi alipostaafu mwaka 2011. Uongozi wake ulichangia sana kuimarisha amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa katika mazingira mapya ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini.

“Ni kwa kutambua kipaji kikubwa cha uongozi alichokuwa nacho Marehemu Jaji Lewis Makame, Taifa letu limepoteza mtu muhimu sana kwani hata baada ya kustaafu kwake alikuwa bado anahitajika sana kutokana na mchango wake wa ushauri katika mambo mengi yanayohusu maendeleo ya nchi yetu”, amesema Rais Kikwete na kuongeza,

“Kutokana na msiba huu mkubwa, nakutumia Salamu za Rambirambi kwa kumpoteza aliyekuwa Kiongozi Mahiri wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kupitia kwako, naomba Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi ziifikie Familia ya Marehemu kwa kumpoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu, Jaji Lewis Makame, Amina”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba huu.

Amewahakikishia Wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa, na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema awape moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira Wanafamilia wote, ndugu na jamaa wa Marehemu, ili waweze kuhimili machungu ya kuondokewa na Mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni Mapenzi yake Mola.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Agosti, 2014

Monday, 18 August 2014

KAMATI KUU YA HALMASHAURI KUU YA CCM KUKUTANA MJINI DODOMA.



Dodoma/Dar. Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM inakutana leo mchana mjini Dodoma chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete huku ikitarajiwa kufanya uamuzi mgumu wa mchakato wa Katiba.

Kikao hicho kinaketi mara ya pili katika muda mfupi, baada ya hivi karibuni kukaa jijini Dar es Salaam na kueleza kuridhishwa na mchakato huo.


Hata hivyo, safari hii kikao hicho kinaketi kukiwa na maswali lukuki ambayo hayajapata majibu: Je, Bunge la Katiba liendelee au livunjwe? Je, lisitishwe kwa muda kupisha maridhiano au la? Je, kuna umuhimu wa maridhiano? Kuna ulazima wa kuwapo Ukawa bungeni?


Akizungumzia kikao hicho, mtaalamu wa sayansi ya siasa na utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema jambo kubwa litakalojadiliwa katika kikao hicho ni kauli tofauti zilizotolewa na wananchi kuhusu mchakato wa kupata Katiba Mpya.


“Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba ameshauri yafanyike maridhiano kwanza na wapo wanaCCM waliomuunga mkono. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema naye ameonyesha wasiwasi wake, Ukawa na Jukwaa la Katiba Tanzania nao wamesema yao. Nadhani kuna jambo CCM wameliona na wanataka kuliweka sawa,” alisema Dk Makulilo.


Aliongeza, “Kujua nini wataamua ni ngumu lakini kutokana na hali ilivyo kwa sasa ni wazi kuwa wanakutana kuona nini kifanyike.”


Kwa upande wake Bashiru Ali alisema, “Tangu mwanzo mchakato wa Katiba haukuwa katika ilani ya CCM, sasa unaweza kujiuliza wanakwenda kujadili nini wakati hata katika mikakati yao ya miaka 10 na 20 ijayo hakuna mpango wa kuandika Katiba.”


Habari zilizozagaa mjini Dodoma zinadai kikao hicho pia kinaweza kupendekeza kuwashughulikia wanachama wake waliotoa kauli zinazopingana na msimamo wa chama hicho.


Miongoni mwa waliotoa kauli zinazopingana na chama hicho ni Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba kutokana na matamshi yake ya kuhoji uhalali wa vikao vya Bunge la Katiba kuendelea bila uhakika wa akidi.


Mbali na Mwigulu pia wabunge kadhaa wa CCM akiwamo, Esther Bulaya (Viti Maalumu), Kangi Lugora (Mwibara), Deo Filikunjombe (Ludewa), Ridhiwani Kikwete (Chalinze) nao wamekaririwa kwa nyakati tofauti wakitoa misimamo inayokinzana na chama chao kuhusu uhalali wa Bunge la Katiba kuendelea bila kuwapo maridhiano na Ukawa.


Hata hivyo, habari nyingine zinasema iwapo kuna mpango huo, Mwigulu anaweza kuondolewa kutokana na utaratibu wa chama hicho kuwaondoa kwenye sekretarieti wajumbe wake wanaoteuliwa kushika nyadhifa serikalini.


Chanzo chetu kinasema ikiwa hilo litatokea kwa sababu ya Mwigulu kuteuliwa Naibu Waziri wa Fedha, basi mpango huo hautamwacha nyuma Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje, Dk AshaRose Migiro ambaye pia hivi karibuni aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na gazeti hili jana, alikanusha kuwapo kwa mpango wa kumwondoa Nchemba katika nafasi yake na kwamba kikatiba kikao chenye uwezo huo ni Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.


“Hizo taarifa ni za uongo kabisa, kikao kweli kitakutana kesho (leo) saa 8:00 mchana chini ya Mwenyekiti Rais Kikwete na ajenda ni moja tu, ambayo ni mchakato wa Katiba. Kikao maalumu huwa na ajenda moja maalumu, hakuna mengineyo wala nini,” alisema Nnauye.


Alisema CC itapokea taarifa kuhusu mchakato wa Katiba unavyokwenda itakayotolewa na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro na baadaye kujadiliwa na wajumbe.


Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana zinasema hatua dhidi ya kiongozi huyo wa juu katika chama zinatokana na kile kinachoelezwa kuwa ni “kuwaudhi makada wa CCM” kutokana na kauli yake hiyo.


Nchemba jana alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kupitia ujumbe mfupi wa maandishi, “Sina taarifa za kung’olewa, nimealikwa kwenye kikao kama NKM (Naibu Katibu Mkuu wa CCM).”


Hata hivyo, ikiwa CCM itafanya uamuzi wa kumwondoa Nchemba, huenda ukapokewa kwa hisia tofauti na umma wa Watanzania ikizingatiwa kwamba pamoja na kutoa kauli zinazokinzana na msimamo wa chama chake, amekuwa akiungwa mkono na wananchi wa kada mbalimbali.


CC ya CCM ambayo hivi karibuni ilibariki Bunge la Katiba kuendelea hadi lifike mwisho, inakutana leo kwa dharura wakati mchakato wa Katiba ukidaiwa kutokuwa na uhalali wa kisiasa kutokana na kususiwa na idadi kubwa ya wajumbe wa Bunge Maalumu ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).


Kutokana na kutokuwapo Ukawa ndani ya Bunge, kuna hofu kwamba Bunge linaloendelea na vikao vyake Dodoma litakosa theluthi mbili ya kura kutoka Zanzibar, hivyo kutopatikana Katiba Mpya.


Kutokana na hali hiyo, Mwigulu amekaririwa mara kadhaa akisema hakukuwa na haja ya Bunge hilo kuendelea na vikao bila kuwa na uhakika wa kutimiza akidi, vinginevyo itakuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma, na wananchi hawatawaelewa.


Kutokana na mazingira hayo, vyanzo vya habari vinasema CCM lazima ifanye uamuzi mgumu wa ama kuziba masikio isisikie kelele za makundi yanayotaka Bunge lisitishwe hivyo iamue liendelee, au igeuke jiwe kwa kulisitisha na kukiuka uamuzi wake wa awali.


Katika siku za karibuni kumekuwa na taarifa kwamba viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakifanya vikao vya siri na wale wa vyama vya upinzani kwa lengo la kufanyia marekebisho Katiba ya sasa ili kutengeneza mazingira mazuri ya uchaguzi mkuu mwakani iwapo Katiba mpya itakwama.


Miongoni mwa maeneo ambayo vyama hivyo viliyaainisha katika vikao vyake vya siri ni pamoja na kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, matokeo ya kura za Rais kuhojiwa mahakamani na mgombea binafsi.




Mwananchi.

Friday, 15 August 2014

HOTUBA YA RAIS JAKAYA KIKWETE KWENYE MKUTANO WA DIASPORA AGOSTI 14,2014 DAR ES SALAAM


KATIBU CCM WILAYA YA MUFINDI NDG. MIRAJI MTATURU NA MAONI JUU YA KATIBA MPYA.


katibu Muenezi wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mufindi Daud Yasini,akizungumza na wananchi wa kinyanambo Wilayani Mufindi


katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mufindi Miraji Mtaturu,akimkabidhi bendera Balozi wa shina namba 15, wakati wa ziara yake Wilayani Mufindi





katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mufindi Miraji Mtaturu, akiwasalimu wanachama wa CCM shina namba 15, wakati wa ziara yake Wilayani Mufindi


                                     
                                                 Na Mathias Canal, Kwanza Jamii-Mufindi

Katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mufindi Miraji Mtaturu,akizungumza na wananchi wa kinyanambo wakati wa ziara yake Wilayani Mufindi

Bila Damu katika mwili wa binadamu ni vigumu sana kuitwa Binadamu kwani ni kiungo pacha katika maisha ya binadamu, Binadamu anapitia hatua kuu tatu awapo duniani ikiwa ni pamoja na hatua ya kwanza ya kuzaliwa, ya pili ni kuoa/kuolewa na mwisho ni kifo.

Katika hatua hizo zote kuna wakati atahitaji kupata elimu juu ya ujairiamali ama elimu yeyote inayoweza kumkomboa kutoka katika utumwa wa fikra finyu.

Nilimnukuu katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mufindi Miraji Mtaturu, alipokuwa akizungunza na wananchi wa Kijiji cha Ndolezi na Kinyanambo, Kata ya Kinyanambo kwenye moja ya mikutano yake inayoendelea kwa ajili ya kuimarisha chama, alipokuwa akizungumzia juu ya mchakato wa upatikanaji katiba mpya unaoendelea kwenye bunge maalumu la katiba Mjini Dodoma,alisema kwamba Katiba ni njia kuu, Wapingaji ni mchepuko kwani hawaoni kama wajumbe wameshatumia fedha nyingi za watanzania hivyo ni lazima katiba ipatikane.

Mtaturu alisema kwamba katiba sio kitabu cha historia kwamba mtu atasoma na kukiweka ndani, bali katiba ni sheria mama ya Tanzania ambayo ndiyo inayowaongoza watanzania hivyo hakuna haja ya kusimamishwa kwa mchakato huo kwa sababu ya matakwa ya wachache wasiopenda maendeleo katika nchi yenye amani na upendo.

Alisema katiba ndiyo ambayo inataja haki zote za wananchi wa Tanzania, hivyo kama watanzania watakubali kuchezewa na baadhi ya wajumbe wa bunge maalumu la katiba ambao wao wameweka mbele maslahi ya vyama vyao na uroho wa madaraka pasipo kutazama na kuwahurumia wananchi ambao ndio wapiga kura wao na ndio wanaoumizwa kwa kupotea fedha zao nyingi hususani pale ambapo hawatapatiwa katiba, jambo hili litakuwa ni utumwa kimwili na hata kiroho.

Mtaturu alisema katiba ya Tanzania imeandikwa mara tatu, mwaka 1961, 1964 na 1977 baada ya hapo katiba imeandikwa kwa viraka viraka mpaka mwaka 2014 ambapo katiba imeanza kuandikwa tena, ambapo mchakato wa kuandika katiba ulianza tangu mwaka 2012 lakini wapinzani wamekuwa wakipinga kila jambo tangu mchakato huu unaanza hadi hivi sasa.

Hata hivyo katibu alisema kuwa tume ya mabadiliko ya katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba, ilizunguka nchi nzima kukusanya maoni ambapo hata hivyo ilikusanya maoni kwa watu 356,000 kati ya watanzania 44,000,000 kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Alisema pamoja na hayo yote maoni ya watu 200,000 hayakuchambuliwa kwani walichambua maoni ya watu 156,000 pekee.


Alisema watu 37,000 pekee ndio walizungunzia mambo ya muungano na watu 26,000 wanataka serikali tatu, hata hivyo watu 19,000 kati ya watu 26,000 wote wanatoka Mkoa wa Kigoma.
Mtaturu alihoji kama mkoa mmoja wa Kigoma unaweza kuwa na nguvu ya kuamua mustakabali wa taifa la Tanzania lenye jumla ya mikoa 30.


Aliongeza kuwa mfumo wa serikali tatu ni mfumo hatarishi kwa watanzania kwani muarobaini wa maisha ya Mtanzania sio kuwa na serikali 3 ambazo zitaongeza gharama ya matumizi ya fedha za wananchi bali kuwa na serikali mbili zenye mtazamo wa kumsaidia mtanzania kujikomboa katika wimbi zito la umasikini ambalo limejiimarisha hapa nchini Tanzania.

TAMKO RASMI LA KATIBU WA HAMASA NA CHIPUKIZI WA JUMUIYA YA UMOJA WA VIJANA WA CCM.




Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Paul Makonda akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa sekretarieti uliopo Ofisi za makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi maarufu kama white house, mjini Dodoma.




                                              TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Demokrasia bila mipaka ni ukichaa na demokrasia bila nidhamu ni uwendawazimu” Mwl Jk Nyerere

Ndugu zangu Watanzania, naomba mfahamu kuwa miongoni mwa wajumbe wote wa bunge la katiba takriban 600, wajumbe waliofanya maamuzi haramu ya kugomea ni 79 ambao ni pungufu ya asilimia 15% ya wajumbe wote, na sio kweli kuwa wao pekee ndio wenye tafsir sahihi ya rasimu. Wajumbe wa makundi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa vyama vyote vya siasa takriban 18 kati ya 22 bado wamo kwenye bunge, kati ya wajumbe wa kundi la 201 walioasi ni 15 ambapo bara ni 9 na zanzibar 6 lakini pia katika wanaojiita UKAWA wapo wabunge ambao wameendelea kurudi bungeni kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa. 
Takwimu hizi zinatuthibitishia kuwa UKAWA ni kikundi kidogo cha watu waliojipanga kuvuruga AMANI ya nchi, watu ambao hawataki KATIBA wala hawataki MUUNGANO.

Ndugu zangu watanzania, naomba leo niwape picha na kilichopo nyuma ya pazia ya kikundi hiki kiitwacho ukawa ambacho kinaratibiwa na viongozi wachache na maslahi yake kujulikana kwa wachache zaidi tena yaliyojikita katika misingi ya kibinafsi. 
 
Mfano, ndoa ya CUF na CHADEMA inayopelekea NCCR mageuzi kuwa bendera fuata upepo imejengwa katika misingi ya kuvunja muungano, kwa makubaliano kuwa CUF kubaki na Zanzibar na CHADEMA kubaki na Tanganyika. CUF inataka inufaike na mkakati dhalimu wa kunyonya rasilimali za wazanzibar yakiwemo mafuta bila kushurutishwa na sheria za muungano kwani wakiamini kubaki na muungano imara CUF na viongozi hao wachache katika chama hicho wanakosa fursa za kupora rasilimali za wazanzibar. Ikubumbukwe Muungano ndio unalinda mipaka na usalama wa raia katika kujiendeleza na kujinufaisha bila ubaguzi wa kikundi cha watu wachache ambacho kinaenda kinyume na utawala wa sheria.
 
Ikumbukwe kuwa rasimu ya CUF walioipeleka kwa Mhe. Raisi mwaka 2011, mapendekezo yao ni tofauti na madai yao sasa ya serikali 3, hapa inatosha kutupa picha kuwa nia yao ni kuvunja muungano ili watuache katika mfarakano kama nchi nyingine zinazoteseka kwa sababu ya wanasiasa uchwara. 
 
Ifahamike ajenda ya CHADEMA ni kuvunja muungano ndio maana CHADEMA hawahangaiki kuimarisha chama Zanzibar, nia yao ni kubaki na Tanganyika ili waigawe Tanganyika katika vipande vipande kwa lugha ya majimbo ili adhima yao ya ukanda na ukabila itimie. Moja ya kanda yao ambayo wametangaza katika kanda 8 walizo nazo ni Kilimanjaro, tanga, arusha na manyara. CHADEMA ina amini kanda hii inajitosheleza kwani ina bandari,bunga za wanyama,madini, milima . Na hii imepelekea mbunge mmoja wapo wa CHADEMA kulazimika kusema kaskazini ni nchi huru huku mwenyekiti wao Mbowe akiendelea kudai mapato ya mlima Kilimanjaro yabaki Kilimanjaro.
 
Katika kipindi hiki ambacho wenzetu wamegomea bunge la katiba ambalo lipo kisheria na madai yao yakibadilika kila kunapokucha tena yakiwa na upotoshaji mkubwa kwa kufanya siasa chafu ili mradi watimize azma ya kuisambaratisha Tanzania wakiwa makuwadi wazuri wa soko huria. Ukihoji leo sababu iliyowafanya watoke bungeni ni tofauti kabisa na sababu waliyoitoa siku wanatoka bungeni, eti msingi wao mkuu wao ni watetezi wa wananchi. Lakini tumesikia katika vyombo mbalimbali wananchi hao wakiwaasa na wakiwataka warejee bungeni ili kukamilisha kazi ya kisheria na tumaini la watanzania la kuwapatia katiba mpya. 
 
UKAWA hawa bila haya wamekataa. Swali..? wanamtumikia nani. Mpaka sasa imepelekea wananchi hao wanaosema wanawawakilisha wameamua wenyewe kuja Dodoma kuendelea kusema kero zao na shida zao ili katiba hii iweze kutoa majawabu, mfano tumeshuhudia makundi ya wakulima, jukwaa la wahariri wa vyombo vya habari, wafugaji na makundi kadha wa kadha yameendelea kutiririka Dodoma. Hii ni picha tosha kuwa UKAWA hawawatumikii watanzania na wameamua kuwahadaa watanzania kwa mgongo wa kuwatetea huku ajenda yao ikiwa maslahi binafsi.
 
Ndugu zangu watanzania tunapowaunga mkono watu wanaoendelea kuligomea bunge la katiba wakati tunajua nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria, na wao ndio wamevunja sheria, tujue kabisa kuwa tunaenda kinyume na utawala bora, ambao umejengwa kwenye msingi wa sheria na demokrasia. Msingi wa demokrasia sio kususa baada ya kushindwa hoja, UKAWA hawataki hoja za wengine na wanalazimisha hoja zao pekee ndizo zikubalike kinyume na msingi wa demokrasia. Na bila haya watu hao wasiojua demokrasia wameendelea kuwashawishi watanzania waingie barabarani huku wakijua kuwa Katiba haipatikani barabarani kama wanahoja kwanini wanaikimbia Dodoma..? Mchakato huu ulianza kisheria na utahitimishwa kisheria, sio matamko ya makuwadi wa soko huria.
 
Miongoni mwa madai yao matatu, (i) Rais avunje bunge (2) kinachojadiliwa Dodoma sio rasimu ya warioba (3) Serikali tatu ndio maendeleo

Kwa ujumla wake, UKAWA wanajua mamlaka ya Rais kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011, sura namba 83 imempa Rais mamlaka ya kuunda tume, kuchagua wajumbe 201, kutangaza na kuitisha bunge na kuzindua bunge la katiba, kupokea katiba inayopendekezwa na kuitangaza kwenye gazeti la serikali.,kwanini wanataka kumlazimisha Rais kuvunja Sheria kwani hayo niliyoyataja ndio ambayo Rais anayo mamlaka ya kisheria kuyafanya katika mchakato huu wa Bunge la Katiba, na ndio maana hata wale wajumbe aliowateua ambao wamegomea Rais hajawatengua.
 
,kinachojadiliwa bungeni ni Rasimu ya jaji warioba na kiko wazi, kwa sababu msingi mkuu wa majadiliano ni Rasimu inayotokana na tume tena kwa mujibu wa Sura namba 83 kifungu cha sheria namba 25/26 na kwa mujibu wa kanuni za bunge kifungu namba 33 (8). Wanajua mamlaka ya bunge na waliohusika kutengeneza sheria hizi pamoja na kanuni waache kuwahadaa watanzania.
 
Jambo la mwisho lenye kusikitisha zaidi ni kung’ang’ania Serikali tatu kana kwamba ndio kilio kikubwa cha watanzania, naomba niulize swali kati ya Muungano na migogoro ya ardhi ni jambo lipi limepoteza maisha ya watanzania wengi na ambalo tunatakiwa kulifanyia kazi ili watanzania wasiendelee kumwaga damu. Kati ya tatizo la ajira na muungano, kati ya afya na muungano, kati ya maji salama na safi na muungano, kati ya elimu bora na muungano, kati ya haki za binadamu na muungano eti watu hawa wanaojiita ukawa kwao muhimu muungano kuliko chochote kile.Watanzania naomba tupime kama ni kweli kuwa hawa ni watetezi wetu au ni makuwadi wa soko huria.
 
Kwa niaba ya watanzania wazalendo, napenda kuiomba serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuwatupia UKAWA jicho la pekee katika kuangalia na kufuatilia kwa ukaribu zaidi nyendo za UKAWA na hata kutuambia ni nani wako nyuma yao kiasi cha kuwa na kiburi cha kupindukia. Wito wa watanzania kwa vyombo vya ulinzi na usalama ni kuwa amani, umoja na uhai wa nchi hii uko mikononi mwao, kwani nia ya UKAWA sio nzuri kwa mustakabali wa taifa hili na lazima wakumbuke USIPOZIBA UFA UTAJENGA UKUTA na pia MAJUTO NI MJUKUU NA HUJA BAADAE. UKAWA wanataka kutengeneza Misri, Afrika ya Kati, Libya, Syria, Sudani Kusini nyingine hapa Tanzania.



Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika


 
PAUL MAKONDA

Katibu , idara ya Hamasa na chipukizi

Jumuia ya vijana chama cha mapinduzi (UVCCM)